Jumanne, 12 Aprili 2016

MSHITUKOOO!!! MADIWANI WA MANISPAA YA SHINYANGA MJINI WABARIKI MRADI WA KUELIMISHA MASHOGA NA MAKAHABA.


Wakati serikali ikiendelea na zoezi la kamata kamata ya wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono /kuuza miili yao ,madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wameriruhusu Shirika lisilo la kiserikali la Rafiki SDO kuendelea kutoa elimu ya UKIMWI kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono “machangudoa” na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao “Mashoga”,
Madiwani hao wamebariki mradi huo uendelee kwa masharti matatu ya shirika hilo kutumia wataalam wa afya kutoa elimu ya Ukimwi ,kutoruhusu ndoa ya jinsia moja na kutowapatia mafuta ya vilainishi vinavyosaidia kupunguza michubuko wakati wa tendo la kujamiiana ili kuhamasisha ngono kwao kama ilivyoripotiwa hapo awali. 
Madiwani waliazimia kuliruhusu shirika hilo jana kwenye kikao cha dharura cha baraza lao likiwa na ajenda moja ya kupata ufafanuzi juu ya shughuli za Mradi wa Shirika hilo la utoaji wa Elimu ya Ukimwi kwa watu hao, baada kutoa tamko la kusitisha shughuli zake kwenye kikao kilichopita, kwamba Shirika la Rafiki linatakiwa litoe ufafanuzi wa kina kuhusu elimu hiyo ili kuepuka kukiuka tamaduni za kiafrika. 
Shirika hilo hapo awali lilizuiwa kufanya kazi zake mwezi Machi mwaka huu na Madiwani hao baada ya kupata taarifa ya kufanya kazi zake kinyemelea kwenye kata zao”bila kushirikisha madiwani” huku kukiwa na madai kuwa wanakusanya Machangudoa na Mashoga na kisha kuwahamasisha kuendelea kuuza miili yao pamoja na kuwapatia mafuta ya vilainishi wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. 
Akitoa ufafanuzi , mkurugenzi wa Shirika la Rafiki Gerald Ng’ong’a, alisema elimu wanayoitoa kwa machangudoa na mashoga ni kuwazuia kuendelea na biashara hiyo na kuwahamasisha kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili wajikwamue kiuchumi. 
“Mimi ni mkristo kamwe siwezi kubadili mila na desturi za kiafrika kwa sababu ya mzungu…mradi huu unatekelezwa katika mikoa 11 Tanzania...ndugu zangu siku zote linapotokea jambo yanazungumzwa mengi,kuna wengine wanakuwa hawaelewi matokeo yake kupotosha jamii”,alisema Ng’ong’a. 
“Naomba radhi kwa taarifa zilizoenezwa hapo awali kuwa tunafanya shughuli ya kuchochea ngono,kutetea mashoga pamoja na makahaba... Nakiri kuwa tulifanya kosa kutotambulisha mradi wetu kwa madiwani na kutoipatia taarifa ofisi ya mkurugenzi ,ninakiri hapo tulikosea ndiyo maana zikaenea kwenu taarifa ambazo ni za upotoshaji”, alieleza Ng’ong’a. 
(Kwa hisani ya Malunde 1 blog.)

Jumamosi, 26 Machi 2016

USAJILI ASASI ZA KIRAIA,MASHIRIKA VIKUNDI WASITISHWA.


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kusitisha mara moja usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti na vikundi mbalimbali vya kijamii kwa lengo la kufanya uhakiki wa uhalali wa kuwepo wa taasisi hizo kisheria.
Ameagiza kuwa uhakiki huo ukamilike ndani ya miezi mitatu (siku 90) kuanzia sasa na orodha kamili ya wadhamini ikiwa ni pamoja na picha zao, anuani ya posta na makazi, na taarifa nyingine muhimu za utambuzi wa taasisi hizo mahali zilipo. 
Taarifa hizo ziwasilishwe Rita na nakala wizarani kwa uhakiki na kumbukumbu.
Dk Mwakyembe alitoa agizo hilo, alipokutana na watendaji na uongozi wa Bodi ya Rita, Dar es Salaam jana kwa lengo la kuboresha utendaji wa Wakala na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Rita ina zaidi ya wadhamini 5,000 walio kwenye vitabu vyao vya usajili.
Aidha, Waziri huyo ameitisha kikao wiki ijayo cha mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na asasi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha taratibu za usajili na uendeshaji na kuboresha mawasiliano baina ya vyombo vya usajili vya dola ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Chanzo cha habari ni blog ya Mpekuzi huru.